Azam Academy yaweka rekodi Kili Stars 

Wachezaji wanne wa Azam Academy wamejumuishwa katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kitakachoshiriki mashindano ya Kombe la Chalenji litakaloanza Novemba 27, mwaka huu nchini Kenya.

Kocha wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amewaita golikipa Aisha Manula, beki Ismail Adam Gambo na viungo Joseph Kimwaga na Farid Mussa Maliki kutoka Azam Academy kuungana na wachezaji wengine na kukamilisha jumla ya wachezaji 23 watakaounda timu hiyo.

Kuitwa kwa wachezaji hao kunawapa nafasi ya kuitumikia timu ya Taifa huku upande mwingine wakikosa mashindano yanayoendelea ya Uhai Cup ambapo Azam Academy ni bingwa mtetezi.

Lakini Uongozi wa Azam FC hauna tatizo na hilo na unafurahishwa kuona vijana wake toka kwenye Academy wakipata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa kama CECAFA Challenge Cup

Wachezaji hao wanaungana na wengine na kufikia idadi ya wachezaji 8 kutoka timu ya Azam FC wanaounda  kikosi hicho cha Kilimanjaro Stars, wengine wanaotoka Azam FC ni Erasto Nyoni, Himid Mao, Salum Abubakar na Said Morad.

Pia inatarajiwa kuwapo kwa baadhi ya wachezaji wa Azam FC kwenye kikosi cha Zanzibar Heroes na Kenya Harambee Stars na kuifanya Azam FC iongoze kutoa wachezaji wengi kwenye mashindano hayo kama ilivyokuwa miaka miwili iliyopita

Kilimanjaro Stars iliyoko katika kundi B la michuano hiyo inatarajia kuondoka Jumatatu (Novemba 25 mwaka huu) kwenda Nairobi kushiriki michuano hiyo inayoshirikisha nchi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wachezaji wanaounda kikosi hicho cha Tanzania Bara ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).

Kilimanjaro Stars ambayo ilitwaa kombe hilo mara ya mwisho 2010, itaanza mchezo wake wa kwanza Nov 28 dhidi ya Zambia katika Uwanja wa Machakos nchini Kenya, mashindano hayo yanatarajiwa kumalizika Desemba 13 mwaka huu.
SOURCE:AZAM WEBSITE

0 comments: