Ripoti kuhusu viwango vya ufisadi Duniani hii hapa
Kumekuwepo na shutuma nyingi za ufisadi kwa nchi mbalimbali kwa miaka na miaka, kwa viongozi na viongozi ambapo hii ndio ripoti kuhusu viwango vya ufisadi.
Nchi ya Afghanistan, Korea ya Kaskazini na Somalia ndio nchi zinazoonekana kuwa na ufisadi mkubwa zaidi Duniani huku Denmark na New Zealand zikiwa ndio nchi zenye ufisadi mdogo zaidi.
Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la kupambana na Ufisadi la Transparency International ambalo limesema kuwa kutokana na ukweli kwamba zaidi ya thuluthi mbili ya nchi zinagubikwa na ufisadi, ni hali ambayo itaathiri ukuaji wa uchumi na kukwamisha vita dhidi ya umaskini na mabadiliko ya tabia nchi.
Linasema karibu asilimia 70 ya mataifa yote ulimwenguni yanafikiriwa kukabiliwa na tatizo kubwa la ufisadi katika sekta ya umma na hakuna moja kati ya nchi 177 zilizofanyiwa utafiti mwaka huu iliyopata alama nzuri, orodha ya kila mwaka ya TI ndicho kipimo kinachotumiwa zaidi kuangazia ufisadi katika vyama vya kisiasa, polisi, mifumo ya mahakama na utumishi wa umma, janga ambalo lina athari juu ya hatima ya maendeleo ya nchi na vita dhidi ya umaskini.
Nchi zilizoorodheshwa katika nafasi za mwisho ni pamoja na Iraq, Syria, Libya, Sudan na Sudan Kusini, Chad, Guinea ya Ikweta, Guinea Bissau, Haiti, na Yemen. Nazo nchi zilizofanya vyema ni Denmark, New Zealand, Luxembourg, Canada, Australia, Uholanzi, Uswisi, Singapore, Norway, Sweden na Dinland.
Rwanda iliyo katika nafasi ya 49 ulimwenguni imetajwa kufanya vyema katika eneo la Afrika Mashariki ikifuatwa na Tanzania iliyo katika nafasi ya 111, Kenya katika nafasi ya 136, Uganda inayokuja katika nafasi ya 140, na Burundi iliyo kwenye nafasi ya 157. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iko katika nafasi ya 154 kwenye orodha hiyo.
Heinrich amesema ufisadi unahusishwa na nchi zinazosambaratika kutokana na migogoro na ambazo serikali haziendeshwi kikamilifu na hivyo watu ni lazima watumie kila mbinu kuendesha harakati zao, kupata huduma, kupata chakula na kuishi.
Mtafiti huyo amesema Afghanistan ambako majeshi mengi ya magharibi yanayoongozwa NATO yanaondoka mwaka ujao baada ya kuwa nchini humo kwa zaidi ya mwongo mmoja, ni hadithi ya kutisha Kwa sababu hawajaona mabadiliko yoyote makubwa. Nchi za magharibi zinawekeza kiasi kikubwa siyo tu katika masuala ya usalama lakini pia zinajaribu kurejesha mkondo wa sheria, lakini bado utafiti wa miaka ya karibuni unaonyesha kuwa idadi ya watu wanaotoa hongo bado ni ya juu kabisa ulimwenguni.
source:milard ayo
0 comments: