Milipuko yarindima leo Zanzibar


Mji wa Zanzibar
Polisi Visiwani Zanzibar wamethibitisha kutokea milipuko mitatu ya mabomu kati ya Jumapili na Jumatatu leo mchana visiwani humo.
Akizungumza na mwandishi wetu Erick David Nampesya, mkuu wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame amesema milipuko miwili imetokea leo katika eneo la mgahawa wa Mercury huku mlipuko mwingine ukiwa umetokea katika eneo la Mkunazini, ikifuatia mlipuko uliotokea jana Jumapili katika eneo la Pangawe.
Mkuu huyo wa Polisi Zanzibar amesema kuwa hakuna vifo wala majeruhi katika matukio yote matatu wala mali iliyoharibiwa, isipokuwa madhara ya kisaikolojia kutokana na hofu na taharuki kutokana na matukio hayo.
Aidha mkuu huyo wa Polisi ameeleza kuwa upelezi unaendelea ili kuwabaini waliohusika katika matukio hayo ingawa hadi wakati huu hakuna mtu au mshukiwa yeyote aliyekwishamatwa kuhusiana na matukio hayo.
Kuhusu hatua za tahadhari kufuatia matukio hayo Kamanda Makame amesema Polisi wanaendelea kuimarisha ulinzi katika sehemu mbali mbali visiwani humo ikiwa ni pamoja na kufanya doria katika maeneo kadhaa na amewaondoa hofu wananchi wa visiwa hivyo kuhusu usalama wao.
source:BBC Swahili

0 comments: