MAZISHI YA MANDELA KUVUNJA REKODI ZA AKINA JOHN PAULO II,NA WINSTON CHURCHIL WAZIRI MKUU WA ZAMANI WA UINGEREZA
Afrika na dunia inatarajiwa kushuhudia kitu kipya katika maziko
ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela (95) aliyefariki
dunia juzi, baada ya kuugua kwa zaidi ya miezi sita.
Serikali ya Afrika Kusini imesema kiongozi huyo
ambaye atazikwa Desemba 15, imeandaa mazishi ya kihistoria
yanayosemekana yatazidi yale ya Papa John 11.
Matukio ya shughuli mbalimbali zinazohusu mipango
ya maziko ya kiongozi huyo maarufu yanatarajiwa kushuhudiwa sehemu
mbalimbali duniani, tofauti na tukio jingine lililowahi kutokea barani
Afrika mbali na kombe la dunia.
Rais Jacob Zuma alisema jana kwamba “Mpendwa wetu
Madiba atazikwa kwa heshima zote za Serikali. Nimeagiza bendera zote za
Afrika Kusini zipepee nusu mlingoti na hiyo itaendelea hivyo hadi
tutakapokamilisha mazishi yake.
Mazishi ya Mandela yanalinganishwa na yale ya Papa
John Paul II mwaka 2005, ambayo yalihudhuriwa na wafalme watano, malkia
sita wa falme mbalimbali na marais wapatao 70 na mawaziri kadhaa,
wakiwamo wafuasi wake zaidi ya milioni mbili. Yanakadiriwa pia kulingana
na maziko ya Winston Churchil aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza mwaka
1965.
Marais wote wa Marekani walio hai wanatarajiwa
kuhudhuria mazishi hayo iwapo afya zao zitawaruhusu kusafiri, pamoja na
Prince Charles wa Uingereza na hata Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Pia
watu maarufu wenye urafiki wa karibu na Mandela akiwamo msanii Oprah
Winfrey wameshathibitisha kuhudhuria.
Changamoto la kiusalama
Kutokana na idadi kubwa ya wakuu wa nchi na watu
maarufu duniani wanaotarajiwa kufika Afrika Kusini, suala la usalama
limeelezewa kuwa changamoto mpya kwa vyombo vya usalama nchini humo.
Afrika Kusini imekuwa moja ya nchi zinazokabiliwa
na matukio ya uporaji na mauaji yanayotokana na idadi kubwa ya wahalifu,
wengi wao wakidaiwa kuwa wahamiaji haramu.
“Huyu ni shujaa wa dunia. Tutafanya mipango ya
mazishi makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa. Nadhani kila nchi itakuwa
imeandaa utaratibu wake wa namna ya kushiriki,” alisema mmoja wa
wanadiplomasia wa Afrika Kusini ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Siku 11 za maombolezo
Serikali ya Afrika Kusini, kwa mujibu wa gazeti la
The Guardian tayari imeweka wazi ratiba ya siku 11 za maombolezo tangu
alipofariki dunia juzi jioni. Japokuwa ratiba hiyo ilishaandaliwa karibu
mwaka mmoja uliopita na kupitiwa na kufanyiwa maboresho katika baadhi
ya maeneo, inaonyesha namna maofisa wa Serikali ya Afrika Kusini
walivyolipa uzito suala hilo na kulifanya kuwa tukio la kukumbukwa
katika historia.
“Mwili wake ulipelekwa kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti kwa
ulinzi wa polisi jana, na tayari mipango yote ya kurusha moja kwa moja
kupitia shughuli hii kupitia televisheni imekamilika,” inasomeka taarifa
ya Serikali.
Taarifa ya Serikali iliyotolewa jana pia ilieleza
kwamba tayari vitabu kwa ajili ya rambirambi vimeshaandaliwa katika
ofisi zote za ubalozi, kwenye ofisi za Nelson Mandela Foundation,
majengo yote ya Serikali na kwenye sehemu ya kumbukumbu ya Mandela huko
Soweto.
Katika siku ya tatu, yaani leo wanadiplomasia wa
nchi mbalimbali waliopo nchini humo watapewa taarifa mjini Pretoria
kuhusu utaratibu wa mazishi ya Mandela na katika siku ya nne, yaani
kesho watu mbalimbali mashuhuri wataruhusiwa kuitembelea familia ya
Mandela.
Katika siku ya tano na ya sita kutakuwa na sala
maalumu ya kumbukumbu ya Mandela itakayohudhuriwa na watu mbalimbali na
viongozi wa makundi yote ya kijamii ambapo mwili wa kiongozi huyo mwenye
historia ya kipekee duniani pia utawekwa mbele ya hadhira.
Tukio hilo litahudhuriwa pia na Rais Jacob Zuma na
zitawekwa ‘skrini’ za televisheni katika baadhi ya kumbi za manispaa na
viwanja vya wazi huko Soweto, Cape Town na maeneo mengine kwa ajili ya
kuwezesha watu wengi kushuhudia shughuli zote za mazishi.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, siku ya nane mwili wa
Mandela utawekwa kwenye jengo la Serikali mjini Pretoria kwa siku tatu
mfululizo, ili kutoa fursa kwa wananchi kuuaga.
“Mwili huo utawekwa katika eneo hilo kuanzia
asubuhi hadi jioni kwa siku zote tatu ukiwa ndani ya jeneza la kioo ili
kuruhusu watu kuuona, kisha utaondolewa kwa ajili ya kuandaliwa kwa siku
inayofuata…
Katika siku ya tisa, Jeshi la Afrika Kusini
litaendelea kusimamia na kutoa heshima za mwisho na kufanya maandalizi
ya mazishi rasmi ya kitaifa kwenye jengo la Union Buildings ambapo
Mandela aliapishwa rasmi kuwa rais wa kwanza mweusi aliyechaguliwa
kidemokrasia mwaka 1994.
Pia shughuli ya kuwapokea wakuu wa nchi mbalimbali watakaoshiriki katika maziko hayo itakuwa ikiendelea.
Katika siku ya 10 baadhi ya mitaa itafungwa ikiwa
ni hatua ya kuimarisha zaidi ulinzi na maandalizi ya mwisho ya eneo la
kuuaga mwili huo kwenye Union Building, ambapo jeshi litakuwa
likikamilisha kuandaa vifaa vyote vitakavyotumika wakati wa maziko yake,
kisha mwili wake utachukuliwa na kwenda kuandaliwa rasmi kwa ajili ya
kuhitimisha maziko.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwili huo utawekwa
rasmi kwenye eneo hilo siku ya 11 na kuwaruhusu wakuu wa nchi na wageni
mbalimbali wa kimataifa watakaokuwa wamefika kumuaga hayati Madiba na
baadaye kuhudhuria mazishi hayo.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba baada ya kutoa fursa
kwa wakuu wa nchi kutoa heshima zao za mwisho safari ya kuelekea
kijijini Qunu ambako ndiko alikozaliwa itaanza siku ya 11 kwa ajili ya
kuupumzisha kwa amani, kazi ambayo itasimamiwa na jeshi.
Taarifa hiyo inaeleza kwamba katika siku ya mwisho, asubuhi
mwili huo utapitishwa katika baadhi ya mitaa kwenye Kijiji cha Qunu
kisha kupelekwa katika eneo la nyumbani kwa Mandela na siyo katika
makaburi ya familia ya Mandela.
Wageni wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi ya Mandela
ni pamoja na Rais Barack Obama wa Marekani na mkewe Michelle ambaye
aliwahi kumtembelea Mandela nchini Afrika Kusini mwaka 2011 pamoja na
binti zake, Sasha na Malia.
Pia rais wa zamani, Bill Clinton na mkewe Hillary
ambao wamekuwa marafiki wa karibu wa Mandela wanatajwa kuwa miongoni mwa
watakaohudhuria maziko yake, pamoja na marais wengine wastaafu wa
Marekani.
Chanzo kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Afrika
Kusini kilisema Prince Charles na Waziri Mkuu wa Uingereza David
Cameron, wamethibitisha kwamba watahudhuria.
Mgogoro wa familia
Moja ya mambo yanayotarajiwa kuibua utata katika
mpango huo wa karibu wiki mbili za maandalizi ya mazishi ni mvutano
katika familia ya marehemu Mandela.
Mjukuu wake ambaye ndiye kiongozi wa familia,
Mandla amekuwa akituhumiwa kufanya mkakati wa kumzika Mandela kwenye
Kijiji cha Mvezo ambako anatambulika kama chifu wa eneo hilo.
Wanafamilia wengine pamoja na serikali ya nchi
hiyo wamekuwa wakidai kwamba eneo linalostahili kuzikwa Mandela ni
Kijiji cha Qunu ambako amekuwa akiishi tangu alipostaafu.
SOURCE:MWANANCHI
SOURCE:MWANANCHI
0 comments: