Baada ya fujo za jana Serikali yaombwa kutofunga misikiti Kenya

Vurugu mjini Mombasa
Utulivu kidogo unasemekana kurejea katika mji wa pwani ya Kenya Mombasa baada ya machafuko kuzuka kufuatia uvamizi wa polisi katika msikiti mmoja ambapo walidai kuwa vijana walikuwa wanapewa mafunzo ya itikadi kali za kiisilamu.
Hata hivyo bado wazazi wengi wanawatafuta watoto wao, baadhi yao wakiwa wadogo wa umri huku baadhi ya vijana wakielezewa kuwa na hamaki kubwa kutokana na hatua ya polisi.
Polisi waliwakamata zaidi ya vijana miamoja waliokuwa wamefika katika msiki wa Musa kuhudhuria kongamano kuhusu mafunzo ya Jihadi wakati ambapo polisi walipata taarifa za mkutano huo na kuuvamia msikiti huo ulio mtaani Majengo.
Watu watatu waliuawa akiwemo polisi mmoja katika siku mbili za vurugu kati ya vijana waisilamu na polisi.
Viongozi mjini humo, wameitaka serikali kutofunga misikiti mwili ya Musa na Sakina inayosemekana kutumiwa na wahubiri wa kiisilamu kueneza itikadi kali za dini ya kiisilamu.
Viongozi hao wanasema kwamba hatua kama hiyo itachochea hali zaidi.
Maafisa wa usalama wanaamini kuwa misikiti hiyo imekuwa kitovu cha mafunzo ya itikadi kali za kiisilamu na pia ni eneo ambalo hutumiwa kuwasajili vijana wanaojiunga na kundi la wanamgambo wa kiisilamu la Al Shabaab nchini Somalia.
Masjid Mussa, lilikuwa eneo la vurugu kati ya polisi na vijana siku ya Jumapili na Jumatatu huku polisi wakiwakamata waumini 130 wa kiisilamu. .
Viongozi hao wakiwemo maseneta, wabunge na waakilishi wa wanawake, walisema kuwa kufungwa kwa misikiti hiyo sio suluhisho la kueneza itikadi kali za kiisilamu.
Viongozi hao walioandamana na wazazi waliwataka polisi kuwaachilia vijana waliokamatwa wakati wa ghasia hizo.

0 comments: