SIKU CHACHE BAADA YA STORY ZA LULU KUPATA MCHUMBA KUSAMBAA, LULU AVUNJA UKIMYA NA KUSEMA HAYA
BINTI anayeshikilia Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike ya Ziff 2013,
Elizabeth Michael maarufu Lulu ameweka wazi kuwa amepata mchumba na
kwamba taratibu za kujitambulisha na mahari vitafuata baadaye.
“Unajua mimi ni binadamu na ili nitulie na
kujiepusha na majanga, ni vyema kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu,
anayenijali mimi na kazi yangu hapo nitasimama na kusema kwamba nimepata
sehemu ya kutulia na kuanza maisha mapya ya uhusiano na ndoa,” anasema
Lulu.
Hata hivyo anasema yeye na mchumba huyo (ambaye
hakutaka kuweka wazi jina lake) wana mikakati mingi katika kuyafikia
maisha ya uhusiano yaliyo wazi na yenye baraka za wazazi.
“Siwezi kukutajia jina kwa sasa itafika wakati
atajulikana tu, hata hivyo bado hatujafikia hatua muhimu ikiwa ni pamoja
na kujitambulisha kwa wazazi na masuala ya mahari na ndoa. Vitu kama
hivi vitafanyika baadaye mwaka huu, hata hivyo wazazi wangu sidhani kama
watakuwa na pingamizi katika hili kwani mimi ni mtoto wa kike na
nimekua sasa,” anasema.
Kuhusu Mama Kanumba Lulu anasema: “Huyu ni mama
yangu hana tofauti na mama Lulu hivyo anajua kila kitu na amenipa baraka
zake zote, yaliyopita si ndwele kinachotakiwa ni kuganga yajayo,
namshukuru mama kwani amenionyesha upendo wa kweli na kunishauri katika
maisha, bila yeye nisingekuwa na ujasiri nilionao sasa.
“Mama Kanumba ni rafiki yangu wa ukweli, ana
mapenzi mazito sana kwangu amekuwa mstari wa mbele kunishauri na kunipa
mwongozo wa maisha ni nini na wapi nilipokosea na natakiwa kufanya nini
ili kuwa na maisha yaliyonyooka,” anasema mwigizaji huyo anayetamba na
filamu ya Foolish Age.
Lulu mwenye miaka 19, anasema haikuwa rahisi kwake
kufikiria kutulia kiuhusiano ila amepewa mwongozo bora unaomfanya
afikirie kufanya hivyo kwa sasa.
“Mimi ni binti na kama ujuavyo nina mapenzi yangu
moyoni, si kazi rahisi kuamua kwa sasa lakini nimepewa mwongozo bora na
kuona nini natakiwa kufanya. Kama binti napaswa kuzingatia maadili, mimi
ni kioo cha jamii, inafika hatua inabidi niishi katika maadili hilo
ndilo ninalolifanya sasa.”
Anasema wazazi wake wamempa baraka zote kuhusu
uhusiano wake wa sasa: “Wazazi wangu sasa wanafahamu kwamba nimepata
mchumba, kwa kweli wamenipa baraka zao zote, pande zote hata Mama
Kanumba. Nimekua sasa na mimi nina uamuzi wangu, ni vema kuangalia
ninataka nini lakini kikubwa wananishauri.”
Anasema wazazi wake hawakubali kila anachokitaka:
“Sina wazazi wa kukubali kila ninachokitaka ila nina wazazi waelewa,
wenye kuangalia jambo kabla hawajaniambia sasa unaweza kuendelea, mama
yangu ni mkali sana, hana mchezo hasa pale anapoona kwamba nayumba
kimaisha,” anasema Lulu.
Kuhusu tetesi zilizoenea kwamba ana uhusiano na
msanii wa hip hop Young Dee, Lulu alikana na kusisitiza kwamba hajawahi
hata kuwa na ukaribu na msanii huyo.
“Nashangaa taarifa hizo watu wanazitoa wapi na
mpaka leo nashangazwa na uvumi ulioenea kwamba tulifumaniwa, usiku ule
nilikuwa sehemu nyingine tofauti kabisa, ukweli ni kwamba sijawahi kuwa
na ukaribu na Young Dee, wala hata kumfikiria kama ninaweza kuwa na
uhusiano naye. Bado, hatulingani kwa kweli,” anasema.
0 comments: